Thursday, 24 September 2015

Hunilishi, Hunivishi

[Kiswahili Kitukuzwe] Kroxti:


Nashukuru nimeyaona mengi. Na anayewinda akipata hufurahi. Keti nikueleze yaliyonipata. Yaliyonijiri. Tajiri vyote anavyo na vilivyo hivyo ndivyo vipasavyo. Maskini hana lakini akipata shida zajieleza. Paza sauti uskizwe; binti mrembo mwenye sauti nyororo. Umenitia wasi tena kwenye pingu za ndoto letu hapo petu na ninalolitafuta zaidi ni jawabu. Yajibu maswali yangu na kwa utaratibu; nitibu yanitiyayo shaka. Nimeduwaa kwenye bahari la penzi lako ila ajuaye vipingo vya mtima wangu ataruzuku haja zangu. Sitathubutu kukupoteza ila kila wakati ufaao ni wangu wa kuuchukua. Tutasafiri tuondoke ulimbukeni na faraja zitakazotuandama zitatupata penye afueni. Tutacheza ufukoni tukiwa na pesa mfukoni. Wananitafuta hawanipati hawajui tuko mbioni. Si lenu, ni letu. Si lako, ni langu. Na asimamaye mbele ya umati tafadhali na aseme kitu cha maana. Kitu cha kweli. Tusiwapoteze wafuasi kwa kuwahifadhi ndani ya ulaghai na bila kuuweka ukweli mbali ya midomo zetu. Asemaye asikike; akikosa arekebishwe.  Umefungua pazia na ukanipata mwangalifu. Sikosi, sikosei. Walisema mtaka cha mvunguni sharti ainame na chini sana kwa kina chako mgongo wangu kwako ntauvunja. Nipe alama ya mshangao na nitakueleza mbona hatujafikia kikomo. Mwenda tezi na omo angalau amepanda meli. Ameuvuta upepo mwanana wa baharini. Na kizimbani akajipata bandarini. Kuwa wangu kipepeo na upae juu zaidi. Na kama mwewe, chochote kile kisikulemee. Nipe njia na nitaifuata. Nikipotea, nyuma ntarejea nijue nilipokosea. Wasafiri hawapotei na wakipotea wamesafiri kwingine. N'takushangaza. Nipe mwangaza niangaze njia yangu hata kwenye giza la kiangazi. Nimekuheshimu na hata kwa miaka arobaini, nitakupata ukiningoja. Saidia, saidia; jina lake Saida. Mtoto karembeka, taji kavishwa. Ninachohitaji ukiwa nacho, usinipe wakati mgumu kukipata, hata bila sababu.

2 comments: